Wewe na mwenzi wako mnakwazana kuliko kufurahishana, kuna mahaba kidogo sana yamebaki kwenye ndoa yenu lakini migogoro mingi. Kila njia ya kuboresha mahusiano yenu imeshindikana na hautaki kuendelea kuishi katika hali hii, unataka mabadiliko na furaha ya mwanzo irudi tena. Uwezo upo mokononi mwenu, unaweza kubadilisha ndoa yako na kuwa na ndoa mpya…na mwenzi wako uliyenaye kwa kufanya mambo kadhaa…
Kabili tatizo lako
Kubali kuwa ndoa yako ina hali mbaya na haipo sawa. Usipoteze muda na nguvu kuhuzunika na kujuta badala yake fikiria furaha na burudiko la moyo ambalo mnalikosa wewe na mwenzi wako kutokana na mifarakano kwenye ndoa yenu. Jambo hili liwe msukumo wa kuhakikisha unafanya jitihada zote ili uweze kuponya ndoa yako.
Bomoa ndoa yako iliyoharibika na uijenge upya
Wakati wana wa Israeli wanajenga ukuta wakati wa Nehemia, walipogundua kuwa wamekosea msingi waliubomoa na kuanza upya. Sababu umegundua kuwa ndoa yako imeharibika, bomoa na anza upya kuujenga msingi na kuisimamisha upya. Simamisha nguzo imara za kuishikilia isianguke tena ambazo ni Kusogea karibu na Mungu kwa maombi, kusoma neno lake na kuhudhuria kanisani; Kila mmoja wenu kuwa tayari kufanya kazi ya kuijenga ndoa yenu pamoja bila kulaumiana au kutegeana; na kuwa na muda wa pamoja kila siku ili kuimarisha uhusiano wenu.
Tubu
Badala ya kumlaumu mwenzi wako kwa matatizo ya ndoa yenu, kubali kuwa wote kwa pamoja mmechangia kuharibika kwake. Wajibika kwa matatizo yako yaliyosababisha kuvurugika kwa ndoa yenu. Kubali kuwa huwezi kumbadilisha mwenzi wako lakini unaweza kubadili mwenendo na matendo yako hivyo mwangalie Mungu akuwezeshe kuwa vile anavyotaka uwe. Kiri na tubu dhambi zako mbele za Mungu na umweleze jinsi gani unavyohuzunika dhambi zako zilivyoharibu uhusiano wako na Mungu pamoja na mwenzi wako. Omba msamaha toka kwa Mungu. Amua kuachana na matendo maovu na kutende mema kwa mume wako na watu wote.
Jadili makosa yenu na kufanya kazi kuyarekebisha
Kaeni chini pamoja na kila mmoja wenu kwa hiyari yake akirimakosa yake yaliyopelekea ndoa yenu kuharibika na kuomba msamaha kwa mwenzake na kutafakari pamoja nini kifanyike ili makosa hayo yasijirudie tena. Jitahidi kuwa ‘positive’ katika majadiliano yenu ili muweze kufikia muafaka ambao utaiboresha na kuijenga upya ndoa yenu. Hakikisha mnafanya kazi ya kuyakabili na kuyarekebisha makosa yenu kwa pamoja ili yasiweze kurudi tena.
Amua kuwa ‘positive’
Hata kama hisia zako kwa mwenzi wako sio nzuri, unaweza kuamua kuwasiliana kwa hali nzuri ‘positive’ ambayo hatimaye itaweza kuboresha hisia zako kwake. Tafuta kufanya mambo ambayo yataonyesha kuwa unamjali mwenzi wako, na ufanye hayo kila siku. Muombe Mungu akusaidie kuweza kuona mambo ambayo utayafurahia toka kwa mwenzi wako na jenga tabia ya kumsifia mara kwa mara. Kuwa na muda wa kuzungumza pamoja kuhusu mambo mbali mbali mnayoyapendelea wote.
Ponywa majeraha ya nyuma
Tafuta kuponywa majeraha ya kihisia yanayosababisha matatizo katika ndoa yako. Kama kuna kitu kilikuumiza zamani mfano kudhalilishwa kwa hali yoyote, kutengwa na wazazi, kukataliwa na mchumba n.k ambacho bado kinakusononesha ndani yako, tafuta namna ya kukuwezesha kupona kabisa ili uweze kuwa huru kuendelea mbele na maisha yako. Kama unaona ni ngumu sana tafuta msaada wa wataalamu wa saikolojia na ushauri ili uweze kuponywa kabisa bila kusahau kwenda mbele za Mungu ili kupata msaada.
Samehe
Amua kumsamehe mwenzi wako yale yote aliyokukosea na umweleze hivyo kuwa umemsamehe kabisa na upo tayari kusahau yote na kuanza upya. Usisamehe kwa kutegemea kitu Fulani, samehe kutoka moyoni.
Timiza mahitaji ya kila mwenzi wako
Zungumza na wenzi wako ujue ni nini hasa anahitaji toka kwako na hakikisha unayatimiza mahitaji yake kwa kadiri uwezavyo. Kuanzia mahitaji ya kiroho, kihisia, kimwili na kiuchumi. Patikana pale anapokuhitaji, saidiana naye shughuli mbalimbali za nyumbali, nenda naye matembezi na pia uwe naye katika wakati anapokuwa na huzuni.
Kuwa Imara na mwenye msimamo
Kama mwenzi wako ametawaliwa na ulevi wa kupindukia au ni mgovi ambaye amefikia hatua ya kukupiga na kukutukana unapaswa kuwa jasiri na imara na kumweleza kuwa ni lazima abadili tabia yake au itakubidi ueleze tatizo lako kwa wazazi au watumishi wa Mungu. Pata nguvu ya kukabiliana na hali hii katika maombi na kamwe usikae kimya pale unapokuwa na mwenzi anayekupiga na kulewa kupindukia. Tafuta msaada kwa wazazi wenu au wakubwa wenu huku ukiendelea kuomba mungu kwa bidii.
yah kaka chopra hapo ni kweli kabisa umetueleza. mungu akuzidishie kwa kutupa fahamu zaidi..
ReplyDeletekaka chopra wewe mtoto mdogo mambo ya kiutu uzima unayajuaje? mmmmmhh haya ni poa kuwa na ujuzi wa kuelimisha wengine!!
ReplyDelete