Kuna wanaume ambao kwa kutokujua wanadhani mwanamke anachohitaji ni ‘fidia’ baada ya kuvunjiwa heshima, hivyo huwa wanawavunjia heshima wake zao na baadae kujitoza ‘fidia’ kwa kuwanunulia zawadi kubwakubwa wanawake hao.
Wanawake huwa wanapokea zawadi hizi, lakini hii haina maana kwamba ndoa itaendelea kuwa ya amani na upendo. Mwanamke hata kama atapewa dhahabu yote duniani, kama atajua kwamba mumewe hamheshimu, ni wazi kwamba hatakuwa na furaha ya ndoa. Miongoni mwa mambo sita ambayo mwanamke akiyakosa huhisi kutindikiwa na kukosa furaha ya uhusiano ni heshima.
Kama haki ya mwanamke hailindwi na mwanaume, hata kama kuna kitu gani, ndoa ni lazima itakuwa ni ya kubahatisha. Mwanume anapokuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa yake, mwanaume anapomzuia mkewe kuamua masuala yake mwenyewe ambayo ni haki yake, kamwe mwanamke hawezi kuridhishwa na hayo na hata kama ndoa imejaa watoto wazuri wenye afya na akili na fedha nyingi zimeipamba nyumba yake.
Kama mwanaume ataonyesha kutojali kuhusu matamanio au ndoto za mkewe kamwe mwanaume huyo asitarajie kuwa mkewe atakuwa na upendo naye. Mwanamke huwa anatamani sana kuona mumewe anajali na kuyapa uzito matamanio au ndoto za mkewe. Kwa mfano mwanamke anapoonyesha kwamba, angependa kuanzisha shughuli labda ya biashara au wangependa wapate mtoto na mwanaume akaonyesha kutojali kuhusu matamanio hayo, kamwe mwanamke hawezi kutulia na kuwa na amani.
Kuna vitu au mambo ambayo mwanamke anayahitaji maishani, mahitaji hayo ni mengi yakiwemo yale ya msingi katika maisha na yale ya kawaida. Inatosha kusema kwamba, mwanamke anapogundua kwamba mumewe hajali juu ya mahitaji yake huwa hajisikii vizuri.
Kwa ujumla tunaweza kusema kwamba mwanamke huhitaji heshima katika utashi na matamanio yake. Anapogundua kwamba utashi na matamanio yake havizingatiwi na mumewe hawezi hata mara moja kumkubali mume huyo. Kumkubali hapa ina maana ya kumkubali na kumtambua.
Hapo ndipo tatizo ambalo ni la upande wa pili huanza. Kwa maumbile mwanaume huwa anataka sana mkewe akimuonyesha kwamba anamthamini na kumtambua. Labda hii inatokana na ubabe wa asili wa wanaume ambapo kila wakati angependa kuona mwanamke akimgwaya na kuonyesha kwamba anamtambua kama ‘mwokozi’ wa aina fulani.
Kama mwanamke anataka kumfanya mumewe amsikilize na kujali matamanio na ndoto zake anachotakiwa kufanya ni kumuonyesha mumewe kwamba anamthamini na kumtambua. Kwa mfano mwanaume anapofanya jambo ambalo hata kama halina faida, lakini halina madhara, inabidi mkewe aonyeshe kuzitambua juhudi hizo na kuonyesha kwamba, mume huyo anajitahidi sana katika kufanya mambo yake.
Mwanaume anahitaji sana kuona mwanamke akimsifu kwa juhudi anazofanya, iwe ni za kitabia au za shughuli. Mwanaume anapokuwa na tabia nzuri, ni lazima mwanamke atafute kila njia ya kumuonyesha kwamba ameitambua tabia yake hiyo, kamwe asimuonyeshe kwamba juhudi anazofanya ni kupoteza muda. Pale ambapo mwanaume huonyesha heshima kwa mkewe kwa kuzijali ndoto na matamanio yake ya kimaisha, huhitaji sana kuonyeshwa kwamba heshima yake hiyo imepokelewa. Kwa kawaida mume anapotimiza wajibu wake lazima mke naye atimize wajibu wake.
Kuna wakati na karibu mara zote, mwanamke huwa anamlaumu mwanaume na mwanaume kumlaumu mwanamke kwa kila mmoja kudhani kwamba mwenzake ndio chanzo cha matatizo. Hii ni kwa sababu wote wawili hawajui namna nadharia hii inavyofanya kazi. Huyu anataka kuthaminiwa wakati hampi mwenzake heshima na huyu anataka kupewa heshima wakati hamthamini mwenzake.
Ili kuondoa kulaumiana huko inabidi kila mmoja ajue wajibu wake, kwani kama mmoja ataanza kumpa mwingine kile anachohitaji ni wazi huyu mwingine atajibu kwa kumpa mwenzake kile kinachomstahili mwenzake ambacho ni heshima.
chopra 0721898979 - 0751898979